Thursday, January 19, 2017

KILIMO BORA CHA VITUNGU

Kilimo Bora cha vitunguu sehemu ya pili; magonjwa yanayoshambulia vitunguu na uthibiti wake.

Posted by Nahoza, S.R  |  at  Alhamis, Januari 28, 2017

      Habari ndugu msomaji wa wetu wa makala za kilimo, Natumaini tunaendelea vizuri na mapambano ya kila siku.  natumaini ukimaliza mfululizo wa makala hizi utakua mkulima hodari wa vitunguu. Kila kitu lazima kiwe na msingi imara, karibu tujifunze wote:
      Katika makala hiyo ya wiki iliyopita tuliweza kuangalia aina za kilimo cha vitunguu, mahitaji muhimu katika kutayarisha shamba, upandaji wa mbegu za vitunguu, matunzo ya vitunguu, namna ya kupata mbegu bora pamoja na aina za vitunguu vinavyolimwa nchini kwa wingi.
       Leo katika makala yetu, tutaendelea na kuangalia katika maeneo mengine muhimu yanayohusika katika suala zima la uzalishaji wa vitunguu na kukupa faida inayotakiwa ikiwa wewe ni mkulima uliyepania kufanikiwa. Kwa kuanza makala yetu, tutaanza na kujifunza magonjwa na wadudu waharibifu kwa vitunguu.

Magonjwa na wadudu waharibifu kwa vitunguu.

      Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea.

Wadudu waharibifu. 



Kuna aina tatu (3) za wadudu wanao haribu zao hili:


1. Viroboto wa vitunguu.

      Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao la vitunguu hapa nchini Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wa mavuno. Wadudu hawa huonekana hasa wakati wa kipindi cha joto.

Dalili za kugundua.


      Majani yaliyo shambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyo kithiri majani yote hugeuka kuwa na tabaka nyeupe au kijivu cheupe na baadaye majani hunyauka kabisa.

Kuzuia.


      Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa kama vile thiodan-35, Parathion nk. Ili kupunguza uvamizi mkubwa, panga upandaji wa vitunguu mapema ili kipindi cha joto kiingiapo zao lako    liwe limekomaa.
      Epuka kupanda zao la vitunguu sehemu iliyo kuwa na mazao aina ya vitunguu kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k. Wadudu wengine waharibifu wa vitunguu ni funza anayekata miche na minyoo ya mizizi. Hawa hupigwa vita kwa kuzingatia mzunguko wa mazao bustanini.

2. Chawa wekundu. (Thrips)

      Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu. (Thrips) ambao wanashambulia majani, Uharibifu uletwao na wadudu chawa, unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha mlipuko wa wadudu.

      Wanashambulia majani kwa kukwarua kwarua na kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa na rangi ya fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.

Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-

  •               Kuweka shamba katika hali ya usafi
  •               Kuondoa magugu shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
  •               Kupulizia dawa ya wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
3. Sota (cutworms)  

      Sota au viwavi wa nondo wanasababisha uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota wanapendelea kula wakati wa usiku na mchana kujificha kwenye ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina.

 Uharibifu huu

      unapunguza sana idadi ya mimea shambani na kuleta upungufu wa mazao.
Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka shamba katika hali ya usafi.

4. Utitiri wekundu (Red spider mites)

     Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha upande wa chini wa majani. Wanafyonza maji kwenye majani na kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea unashindwa kutengeneza chakula na baadaye inakufa.

Njia ya kudhibiti:-

  •         Kupulizia dawa za wadudu Karate na Selecron.
  •         Kuteketeza masalia ya mazao .  
  •         Kutumia mzunguko wa mazao.
5. Vipekecha majani (leaf miner)

       Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na kutengeneza mitandao wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.

Njia ya dhibiti:

  •        Kupulizia dawa ya wadudu kama karate Selecron na Dursban
  •        Kuteketeza masalia ya mazao
  •        Kutumia mzunguko wa mazao
Magugu.

      Miche ya vitunguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen

(Goal 2E).

     Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali. Dawa Inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikizwa miche shambani. Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu. Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au kubabua vitunguu.

Magonjwa ya vitunguu.

a)     Ukungu mweupe
     Ugonjwa huu hujionyesha kipindi cha baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mwingi hewani.

Dalili za kugundua Ugonjwa huu

  •        Utaona unga wa rangi ya zambarau katika majani.
  •        Majani hugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kunyauka.
  •        Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na kusababisha kuoza kwake.
Kuzuia

  •         Inashauriwa kubadili aina ya zao katika shamba lako kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii ya vitunguu. Kilimo cha mzunguko wa aina mbalimbali za mazao upangwe kiasi kwamba vitunguu visipandwe eneo moja mpaka baada ya miaka 3 kama ugonjwa ulikuwa mwingi.

  •         Tumia dawa za kuzuia ukungu. Hii ifanyike kabla ya kuona dalili za ugonjwa kwenye vitunguu. Piga dawa kama vile maneb, Dithane M45, zineb ya unga, n.k. Wakati unapoona hali ya hewa inayo wezesha kuenea kwa ugonjwa huu (yaani baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mara kwa mara). Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku sita ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa. Ugonjwa ukisha ingia kwenye mimea hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponyesha.
b) Ukungu wa kahawia

       Ugonjwa huu unaweza kuleta madhara makubwa wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vikiwa katika ghala.

Dalili zake

     Vikovu vya mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye hutoa doa la rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au shina la kitunguu. Baada ya wiki kama tatu hivi tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na kukauka. Ugonjwa huu hushambulia vitunguu hata baada ya kuvuna kwa kupitia shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu,
kidonda au mkwaruzo.

Namna ya kuzuia

      Katika bustani, mara uonapo kitunguu chenye dalili za ugonjwa huu, ondoa mimea na kuiteketeza kwa moto ili kuzuia au kupunguza kuenea kwa ugonjwa.
  •        Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M 45 na dawa zingine za kuzuia magonjwa ya ukungu. Dawa hizi zitasaidia kupunguza kutawanyika kwa ugonjwa.

  •       Tumia kilimo cha kuzungusha au kubadilisha mazao katika eneo la bustani yako. Usipande mfululizo jamii yoyote ya vitunguu katika shamba ulilovuna vitunguu.

  •       Wakati wa kuvuna, epuka kukata au kusababisha vidonda katika vitunguu, yaani vuna kwa kung’olea na siyo kwa kuchimba na jembe.

  •        Baada ya kuvuna anika vitunguu juani kwa siku moja au mbili kabla ya kuviweka katika magunia au ghala.
c) Ugonjwa wa kuoza mizizi
      Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na unasababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu.

Dalili

      Dalili za ugonjwa huu ni mizizi kugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kuwa zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi hufa kwa kunyauka.
Majani nayo hugeuka kuwa na rangi ya njano na kisha shina au mche mzima hunyauka.

Kuzuia
  •         Tumia kilimo cha kuzungusha mazao badala ya kupanda vitunguu katika eneo moja toka msimu moja hadi mwingine.

  •         Panda aina za vitunguu zinazo vumilia ugonjwa huu kwa mfano: Excel, L 36, Granex, White Granex na red creole.
Kumbuka tumejifunza kuanzia utayarishaji wa shamba na aina za mashamba, pili tukaangalia aina za mbegu na jinsi ya kuchagua mbegu bora yenye kustahimili magonjwa na hali ya hewa, pia tukalenga kwenye maeneo na hali ya hewa, tukaangaza na katika Magonjwa yanayoweza kuathiri zao la kitunguu pamoja na kudhibiti wake.
     Ahsanteni.

Sunday, January 15, 2017

KILIMO BORA CHA VITUNGUU

Kilimo Bora cha vitunguu; Maandalizi Ya Mbegu, Shamba Na Upandaji Wa Miche.

Posted by Nahoza, S.R  |  at  Sunday , January 15, 2017

Habari ndugu msomaji wa wetu wa makala za kilimo, Natumaini tunaendelea vizuri na mapambano ya kila siku. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha bora cha vitunguu, na tutaanza kufahamu vitu vya msingi kwanza, na natumaini ukimaliza mfululizo wa makala hizi utakua mkulima hodari wa kitunguu. Kila kitu lazima kiwe na msingi imara, karibu tujifunze wote:


UTANGULIZI

Vitunguu ni zao la pili ambalo hutumika karibu kila siku katika mlo wa familia za kitanzania. Afrika Mashariki, na Dunia Nzima.
Vitunguu vina chukua nafasi kubwa katika matumizi ya mboga hasa kwa wakazi wa mijini. Vitunguu hutumika katika kutengeneza kachumbari, kiungo cha mboga, nyama na samaki. Majani ya kitunguu hutumika kama mboga. Vitunguu pia hutumika kutengeneza supu n.k

Aina Za kilimo Cha Vitunguu
Kilimo cha vitunguu kinaweza kufanyika kwa aina mbili

  •       Green House
  •       Shambani
Kilimo cha kitunguu Green House

Kilimo cha vitunguu katika shamba la kawaida.
 
Mahitaji muhimu katika kuzalisha zao la vitunguu

Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa vitunguu.

Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha. Udongo unao ruhusu mizizi kupenya kirahisi, unao hifadhi unyevu kama vile udongo wa mfinyanzi tifutifu.

Kutayarisha shamba

Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa
vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya
umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au
majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.

Upandaji wa mbegu za vitunguu

Mbegu zinaweza kupandwa kwa mstari au kwa kutawanya katika tuta la kitalu. Katika upandaji wa mstari, mbegu hupandwa katika nafasi ya cm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari. Baada ya kupanda, mbegu hufunikwa kwa udongo na baadaye kwa kuweka matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota, matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli mimea michanga. Mbegu huota baada ya siku 7 hadi 10.

Matunzo ya bustani ya vitunguu

    Umwagiliaji


 Zao la vitunguu linahitaji maji ya kutosha katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa kutunga tunguu. Katika kipindi kisicho na mvua (mwezi mei hadi Agosti) Umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki kwa udongo wa mfinyanzi tifutifu na vitunguu vilivyopandwa katika vijaruba. Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu unashauriwa kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia taratibu kadri zao linavyo kua.

Pia ni vizuri uache kumwagilia maji mapema wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu. Kuthibiti magugu na kupandishia udongo Kitunguu ni zao lisilo weza kushindana na magugu. Magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa vitunguu. Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kutolewa kwa njia ya kutifulia kwa jembe dogo, kung'olea kwa mkono na pia kwa kutumia madawa ya kuua magugu.

Kama unaondoa magugu kwa kutifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu ili kutoharibu mizizi na vitunguu vyenyewe, kwani mizizi ya vitunguu ipo juu juu sana. Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kuwa mashina ya vitunguu vyako ndani ya udongo kama sentimita 5. Pia kuna aina ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo wakati vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana.

Hali ya hewa na maji

Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu.

Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji. Maji mengi hasa
wakati wa masika inasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa
vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu sana wakati
wa kukomaa na kuvuna vitunguu.

Aina za vitunguu

Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia 40-60kgs kwa hekta. ikiwa kilimo bora kitazingatiwa. Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia:-

  •     Mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
  •     Msimu wa kupanda
  •     Uwezo wa kuzaa mazao mengi
  •     Uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Mbegu bora

Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesi baada ya kuvunwa (mwaka1). Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo:-


  •     Uotaji zaidi ya 80%
  •     Mbegu safi zisiyo na mchanganyhiko
  •     Zimefungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unyevu.

Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo:

  •     Chanzo cha mbegu
  •     Tarehe ya uzalishaji
  •     Tarehe ya kuisha muda wa
  •      Kifungashio cha mbegu.

Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja
Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama:

  •      ALPHA Seed Co, Popvriend,
  •     · Rotian Seed,
  •     ·  Kibo Seed,
  •     ·   East African Seed Company nk.


 Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA, na maduka ya pembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.
Nikutakie siku njema na kilimo bora, katika makala ijayo tutaangalia magonjwa yanashambulia vitunguu na jinsi ya kuweza kuyazuia.
  
Ahsanteni.

kILIMO BORA CHA NYANYA (TUNGULE)

Kilimo Bora cha Nyanya; Maandalizi Ya Mbegu, Shamba Na Upandaji Wa Miche.

Posted by Nahoza, S.R  |  at  Sunday, January 15, 2017

Habari ndugu msomaji wa wetu wa makala za kilimo, Natumaini tunaendelea vizuri na mapambano ya kila siku. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha bora cha nyanya, na tutaanza kufahamu vitu vya msingi kwanza, na natumaini ukimaliza mfululizo wa makala hizi utakua mkulima hodari wa nyanya. Kila kitu lazima kiwe na msingi imara, karibu tujifunze wote:

UTANGULIZI
 Nyanya ni aina ya mboga inayo zalishwa kwa wingi sana
duniani. Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao
ya mboga linalo limwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na
mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika kila mlo.
Nyanya ni zao umuhimu kama chakula na pia kama
zao linalomwingizia kipato mkulima.

HALI YA HEWA INAYOFAA KWA KILIMO CHA NYANYA
Mahitaji ya zao la nyanya
Nyanya hustawi vizuri kwenye maeneo ya joto, yasiyo na
ukungu mwingi hasa wakati zao linatoa maua na matunda. Zao
hili hupenda kipindi kirefu cha jua na joto ili kuongeza ukuaji wa
matunda na kupunguza magonjwa ya aina ya ukungu/kuvu. Zao
hili halipendi mvua nyingi ingawa linahitaji maji kwa wingi.
Katika kipindi chenye mvua nyingi na jua kidogo nyanya
hushindwa kutoa maua na matunda ya kutosha bali huweka
majani mengi. Katika kipindi hiki pia, nyanya hushambuliwa
sana na magonjwa ya ukungu.

UDONGO UNAOFAA KWA KILIMO CHA NYANYA
Nyanya hupendelea udongo unaopitisha maji kwa urahisi na
wenye rutuba ya kutosha na hivyo hupenda samadi. Udongo
uwe umetifuliwa vya kutosha kuruhusu mizizi kushika vema.

AINA ZA NYANYA
Kuna aina kuu mbili za nyanya kulingana na ukuaji wa mmea:
yaani:
1=> Nyanya zinazorefuka zenye kuhitaji egemezi (mfano
Money maker)


2=> Nyanya fupi zenye kutoa matawi
mengi mfano Roma,Tanya na Cal J.




 KIASI CHA MBEGU
kwa ekari moja utahitaji Mbegu gram 100-150 kwa OPV variety, na Gram 30-50 kwa hybrid (F1) . Gharama za kutosha eka moja kwa OPV variety ni tsh 100,000-180,000, na kwa Hybrid (F1) Gharama ni kati ya tsh 200,000-400,000 kutegemea na aina yenyewe ya mbegu.

UKUZAJI WA MICHE YA NYANYA
Miche ya nyanya huzalishwa kwenye kitalu kwa kupanda
mbegu. Mbegu za nyanya huota baada ya siku 5 hadi 10.
Baada ya kukua kitaluni kwa muda wa wiki 4 hadi 5 toka kuota
kwa mbegu, miche hupandwa shambani. Kabla ya kupandikiza
shambani miche huandaliwa kwa kupunguza umwagiliaji maji
kwa siku moja au mbili ili miche izoee hali ngumu kabla ya
kuhamishiwa shambani.
Hapo shambani miche hupandikizwa kwa kuzamishwa katika
kina kirefu zaidi ya ilivyo kuwa kitaluni. Hii inasaidia miche kutoa
mizizi ya pembeni mingi zaidi kwa ajili ya kufyonza maji pamoja
na virutubisho aridhini. Baada ya kupandikiza mwagilia maji ya
kutosha. Usimwagilie maji juu ya mche wa nyanya. Katika
kipindi cha jua kali, tandaza nyasi kwenye tuta ili kupunguza
upotevu wa maji na unaweza kuweka kivuli kwa kutumia majani
ya miti au migomba.
Kulingana na aina ya nyanya na rutuba ya udongo, nafasi ya
kupandia ni sm 60 kati ya mstari hadi mstari na 45 hadi 60
nafasi ya mche hadi mche AU sm 90 kwa 50 AU 75 Kwa 40.  Kama udongo hauna rutuba ya
kutosha inapendekezwa kutumia nafasi kubwa ya kupanda.
Utunzaji wa zao la nyanya
Nyanya fupi zisizo refuka kwenda juu, ni rahisi sana kutunza na
hazihitaji huduma nyingi. Tatizo kubwa ni kuwa kwa kutambaa
chini, katika kipindi cha mvua huwa karibu na magonjwa
yatokanayo na udongo. Katika kipindi cha jua kali, matunda
huungua kwani mmea huwa na majani machache tu yanayo
kinga matunda yasipigwe na mionzi ya jua.

MBOLEA
Licha ya mbolea ya kupandia, unashauriwa kuongeza mbolea
kipindi cha wiki mbili au tatu baada ya kupandikiza miche
bustanini. Mbolea hii ya kukuzia iwekwe kuzunguka shina la
mmea kwa umbali wa sentimeta 5 hadi saba kutoka kwenye
shina. Kwa mbolea kama vile CAN, NPK, au SA tumia kifuniko
kimoja cha soda kwa shina. Mbolea hii inaweza kuwekwa mara
mbili kabla ya mvuno wa kwanza.
Ili kurefusha kupindi cha uzaaji wa zao la nyanya (na hata
mazao mengine  yatoayo matunda kama vile nyanya chungu,
biringanya, pilipili hoho, nk) inapaswa kuongezea mbolea katika
kipindi cha uvunaji mfano baada ya kuvuna mara mbili
unashauriwa kuongeza mbolea ya samadi na mbolea kama vile
NPK. Hii inasaidia mmea kuendelea kutoa maua bila kuchoka.
Kwa kawaida nyanya fupi jamii ya “Roma” huweza kuzaa na
kuvunwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8 tu. Lakini kama utakuwa
unaongezea mbolea na kukazania matunzo ya bustani (hasa
usafi wa bustani na kumwagilia maji ya kutosha), nyanya
zinaweza kuendelea kuzaa kwa muda mrefu zaidi. Hii ni tofauti
na mazoea ya wakulima wengi kuwa mara nyanya zianzapo
kuzaa huduma za palizi na usafi wa shamba huachwa na kutilia
maanani kazi ya kuvuna pekee. Hii inajitokeza zaidi kwenye
aina ya nyanya fupi.
Kwa nyanya fupi ni vizuri kuhakikisha kuna matawi mengi
iwezekanavyo ili kuweza kupata matunda mengi zaidi. Hivyo
usipunguze matawi katika aina hii ya nyanya.
Kwa nyanya ndefu zenye kuhitaji egemezi,tunashauriwa kukuza
nyanya kwa tawi moja lisilo na vichipukizi pembeni au matawi
mawili na kuacha mnyanya urefuke.
Kupunguza majani ni muhimu pia katika kupunguza
maambukizo ya ukungu katika shina na pia kutoa nafasi ili
mwanga kupenya na kuruhusu mzunguko wa hewa. Majani
yapunguzwe kipindi cha asubuhi kwa kutumia mkono na siyo
kisu kwani kinaweza kueneza magonjwa kutoka mche hadi
mche.
Kwa nyanya ndefu, majani ya chini ya matunda huondolewa
kadiri unavyo endelea kuvuna. Unashauriwa upunguze majani
wakati wa asubuhi kwa kutumia mkono na pia usitoe zaidi ya
majani matatu katika mmea kwa mara moja.

UMWAGILIAJI WA NYANYA
Nyanya ni zao linalohitaji maji mengi sana kwa ajili ya ukuaji wa
mmea na matunda yake. Umwagiliaji uwe wa kulingana kwa
kila siku iliyo pangwa. Usibadilishe ovyo kiasi cha maji na ratiba
ya kumwagilia. Hii inasababisha kuoza kwa kitako cha nyanya.
Pia ili kutunza maji katika udongo, inashauriwa kuweka
matandazo katika mzunguko wa shina la nyanya au bustani
yote. Nyanya inayo kua vizuri hutumia maji lita mbili kwa siku
katika kipindi cha jua kali. Hivyo katika umwagiliaji ni busara
kuzingatia kiasi hiki cha maji katika kipindi kama hiki. Pia kama
unatumia keni, mpira au bomba usimwagilie maji juu ya matawi
ya nyanya kwani umwagiliaji wa namna hii utasababisha
kuenea kwa magonjwa ya ukungu.

CHANGAMOTO ZA KILIMO CHA NYANYA
Matatizo yanayosumbua kilimo cha zao hili ni magonjwa na
wadudu waharibifu. Hapa tutajifunza mbinu mbali mbali za
kuzuia magonjwa na wadudu waharibifu.

WADUDU WAHARIBIFU WA NYANYA
 {i} Funza washambuliao matunda
(Funza wa vitumba)

Huyu funza hushambulia mazao mengine kama vile pamba,
mahindi, mtama, maharage n.k. Mdudu huyu hushambulia
matunda ya nyanya kwa kutoboa na hivyo kuyafanya yapoteze
soko kwasababu hayafai kuuzwa katika soko na pia yanaweza
kuoza wakati wa usafirishaji.
Ili kuthibiti piga dawa ya kuua wadudu kama vile thiodan, sevin
ya unga, karate, selecron, n.k. Muarobaini hutumika pia katika
kupunguza uharibifu wa mdudu huyu.

 {ii} Inzi weupe
Wadudu  hawa huruka ruka kwenye shamba la nyanya na kukaa
chini ya majani. Mdudu huyu hueneza magonjwa ya virusi kama
vile “ukoma wa nyanya”. Usafi wa shamba na mazingira ya yake ni
muhimu katika kupunguza kuzaana kwa wadudu hawa.

Ili kuthibiti wadudu hawa kwenye bustani ya mboga na pia
katika maficho yao, piga dawa kama vile karate,
cypermethrin mara kwa mara.

Panda mimea mingine (kama vile tumbaku) inayo vutia
wadudu hawa kwenye maeneo ya bustani kisha piga dawa
katika miche ya tumbaku ili kuwaangamiza kwa wingi.

 {iii} Minyoo
Mdudu huyu hukaa kwenye udongo wenye
unyevu wa kutosha. Huvamia mizizi ya nyanya na
kuharibu mfumo wa usafirishaji maji na chakula
kwenye nyanya iliyo athirika. Uking'oa mche wa
nyanya utaona vifundo kwenye mizizi.
Kuzuia
Mbinu za kuthibiti ongezeko la wadudu hawa ni kuharibu hali ya
udongo inayo mfanya aishi na kuzaana. Mbinu hizi ni:

Kulima shamba kwa kutifua baada ya kuvuna nyanya ili
udongo wa chini ukae juani na kukauka. Hii inasaidia
kuangamiza wadudu hawa kwa joto na ukosefu wa maji.

Choma moto na kuteketeza mabaki ya nyanya baada ya
kuvuna.

kuzungusha aina ya zao la nyanya au jamii ya nyanya na
mazao mengine yasiyo vamiwa na adui huyu. Hii
huwafanya minyoo wasipate hifadhi na chakula kutoka
kwenye mimea wanayo tumia kuishi na kuzaliana. Hivyo
idadi yao kupungua katika udongo.

kabla ya kupanda zao weka samadi nyingi katika udongo
kwenye eneo lililo athiriwa na wadudu hawa kwani
hawapendi udongo wenye samadi nyingi.

Panda manung'a nung'a (
Tagetes spp
) katika eneo
lililoathirika na minyoo hawa, mimea hii hutoa sumu ya
aina fulani ambayo huathiri ukuaji na kuzaliana kwa
minyoo hawa.

MAGONJWA YA NYANYA
Uchunguzi umeonyesha kuwa  nyanya na mazao mengine jamii ya nyanya ndiyo
hushambuliwa sana na magonjwa kuliko mazao mengine ya
mboga.

 {i} UKUNGU
Huu ni ugonjwa unaopenda hali ya unyevu mwingi hewani.
Hivyo hujitokeza zaidi wakati wa masika. Pia sehemu zenye
umande mwingi  wakati wa usiku, ugonjwa huu hujitokeza hata
wakati wa kiangazi
Dalili za ukungu katika nyanya
Ugonjwa huu hushambulia shina, maua na matunda. Kuungua
kwa majani kama vile yamechomwa na maji moto. Chini ya jani
utaona unga unga mweupe. Matunda pia hushambuliwa na
ugonjwa huu na hugeuka kuwa meusi na magumu.
Kuzuia

Inabidi kuchanganya mbinu mbali mbali za kupambana
na ugonjwa huu.

Kwanza ni usafi wa shamba kwa ujumla yaani
hakikisha unaondoa magugu katika bustani.

Tandaza nyasi juu ya matuta yaliyo pandwa nyanya.

Ondoa majani yaliyo zeeka na yanayo onyesha dalili za
ugonjwa huu. katika kupunguza majani, hakikisha
sehemu za chini ya mmea ni wazi na kuna mzunguko
mzuri wa hewa. Punguza majani katika mmea ili
kupunguza umande na ukungu kwenye mmea.

Baada ya kupunguza majani na machipukizi hakikisha
unatupa mbali majani hayo na siyo kuyaacha kwenye
tuta la bustani.

Ondoa kabisa mmea ulio na dalili za ugonjwa huu

Kupiga dawa katika kipindi cha mvua mara baada ya
mvua kubwa. Fanya hivyo mara moja au mara mbili
kwa wiki kutegemea na wingi au mfululizo wa mvua.
Unapoona jua limetoka piga dawa ili ugonjwa
usijitokeze tena.
Baadhi ya madawa yanayofaa kukinga ugonjwa huu ni Dithane
M45, Bravo, Benlate , Ridomil, Topsin n.k. Kumbuka kuwa kila
mwaka madawa yenye nguvu zaidi hutengenezwa, hivyo uliza
watalaam walioko karibu nawe. Ingawa Blue Copper inauzwa
kwa bei nafuu, nguvu yake in kidogo sana kuthibiti huu
ugonjwa.
Muarobaini pia unaweza kutumika kupunguza ugonjwa huu.
Changanya unga unaotokana na mbegu za muarobaini kiasi
cha nusu kilo ya unga katika lita 20 za maji.

 {ii} Ugonjwa wa ukoma wa nyanya
Huu ni ugonjwa wa virus unao enezwa na inzi mweupe. Inzi
hawa hushambulia zaidi nyanya wakati wa kiangazi, hasa
kipindi cha joto kali.
Dalili

Majani machanga hujikunja na baadaye majani yote.

Kupungua kwa utoaji maua na matunda na hata
yakitokea matunda huwa ni madogo.

Mmea kudumaa na kutozaa kabisa.
Kuzuia
Mbinu madhubuti ni kupunguza kuenea kwa ugonjwa huu
kwenye shamba kwa kudhibiti kuzaana na kuenea kwa mdudu
(inzi mweupe) kama tulivyo ona katika kupambana na mdudu
huyo, yaani:

Kuondoa mimea michache iliyo shikwa na ugonjwa
maana wadudu hawa wanachukua ugonjwa huu kutoka
mimea hii.

Kutumia mbegu zilizo hakikishwa kuwa zinaweza
kuvumilia ugonjwa huu na kutoa mavuno mazuri.

Usilime nyanya karibu na eneo lililo na mazao kama
bamia,mipapai maana mimea hii huhifadhi inzi
mweupe.

Kuua inzi weupe wanaofyonza nyanya na kusambaza
virusi kwa kutumia madawa. Tumia madawa kama vile
Selecron, Decis, Karate n.k.

Epuka kuchanganya zao la nyanya na mazao mengine
yanayohifadhi hawa nzi kama vile mipapai  na bamia.

Ng'oa na kuchoma moto mimea yote iliyougua ugonjwa
huu.

 {iii} Ugonjwa wa mmea wa nyanya kuoza sehemu ya shina
inayogusa udongo na mmea kunyauka kama vile umekosa
maji

Wadudu wanaosabisha ugonjwa huu hupatikana ardhini.

Hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huu baada ya dalili
kujitokeza.

Kupiga madawa za viwandani ardhini kabla ya kupanda
nyanya husaidia kupungu wadudu wa ugonjwa.

Epuka kupanda nyanya au mazao jamii ya nyanya katika
eneo moja kwa muda mrefu mfulilizo . Baadhi ya mazao
yanayohusiana na nyanya ni bilinganya, pilipili, ngogwe,
mnavu, n.k.

{iv} Ugonjwa wa miche michanga ya nyanya kuoza sehemu ya
shina inayogusa udongo na kufa ghafla
Ugonjwa huu hushambulia miche kitaluni na husabishwa na
wadudu waishio ardhini. Mara baada ya dalili, ugonjwa huu
hauna dawa ila unaweza kukingwa kwa kutumia njia zifuatazo:

Choma moto udongo wa kutengezea kitalu kabla ya
kupanda mbegu zako. Kutumia mboji husaidia kukinga
miche dhidi ya ugonjwa huu.

Epuka kumwagilia maji kupita kiasi na kutumia kuvuli
kizito.

{v} Matunda ya nyanya kuoza kitako.
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na:

Umwagiliaji wa nyanya bustanini usio na mpangilio
maalumu. Mfano, kumwagilia mimea maji mengi kisha
kuiacha bila maji kwa siku kadhaa.


{vi} Upungufu wa virutubisho aina ya chokaa.
Dalili zake ni matunda ya nyanya kuoza sehemu ya kitako na
kuonyesha rangi nyeusi.
Kuzuia ugonjwa huu, zingatia kuwa na utaratibu mzuri wa
kumwagilia maji ambao haubadiliki ovyo kiratiba na kiasi cha maji
yanayowekwa. Rutubisha mimea kwa madini ya chokaa kwa
kutumia mbolea aina ya CAN zenye madini haya.

UVUNAJI WA NYANYA
Nyanya  za kupelekwa sokoni zinabidi ziwahi kuvunwa mara tuuzinapoanza kuiva ili kuzifanya ziwe salama kipindi cha kusubiri kuuzwa na kusafirishwa.
Nyanya zinazopelekwa viwandani zinatakiwa zivunwe baada ya kukamilika uivaji wake.Ili kuzisafirisha nyanya vizuri tumia maboksi ya mbao.
   Ahsanteni

Friday, January 13, 2017

first post

Kilimo Bora cha Nyanya; Maandalizi Ya Mbegu, Shamba Na Upandaji Wa Miche.

Posted by Nahoza S . R |  at  Friday , January 13, 2017

Habari ndugu msomaji wa wetu wa makala za kilimo, Natumaini tunaendelea vizuri na mapambano ya kila siku. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha bora cha nyanya, na tutaanza kufahamu vitu vya msingi kwanza, na natumaini ukimaliza mfululizo wa makala hizi utakua mkulima hodari wa nyanya. Kila kitu lazima kiwe na msingi imara, karibu tujifunze wote:



Utangulizi:

  •     Nyanya ni zao la mboga ambalo hulimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Inahisiwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru/Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu.

SOMA; Fursa katika Kilimo cha Bustani

Uzalishaji wa nyanya duniani na hapa Tanzania

Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na USA, Italia na Mexico. Kwa upande wa Africa nchi zinazo lima ni kama; Malawi, Zambia na Botswana.

Zao hili hulimwa pia katika nchi za Africa Mashariki, ikiwemo Kenya, uganda na Tanzania.

Zao la nyanya linalimwa karibu maeneo yote ya Tanzania. Uzalishaji wa nyanya ni mkubwa kuliko mazao mengine ya mbogamboga yanayolimwa hapa Tanzania, uzalishaji wa nyanya kwa mwaka ni jumla ya tani 129,578 ikiwakilisha asalimia 51 ya mazao yote ya mboga. Kwa mujibu wa Wizara ya kilimo ya Tanzania maeneo yanalolima sana nyanya ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro (Hai, Moshi na Rombo), Arusha (Arumeru), Morogoro (Mgeta), Tanga (Lushoto), Mbeya (Mbeya vijijini) na Singida. Morogoro ndiyo inayoongoza kwa kilimo hichi ikiwa na wazalishaji wenye zaidi ya hekta 6,159 (ekari 15,398). Pamoja na kwamba eneo la uzalishaji linaongezeka kwenye maeneo mengi lakini uzalishaji wa nyanya bado ni mdogo sana.

Uzalishaji mdogo unasababishwa na kupungua kwa rutuba ya ardhi, upepo, joto, ukame. Sababu nyingine ni pamoja na ukosefu wa aina za nyanya zenye mavuno mengi amabazo zinahimili mazingira ya kwetu, wadudu, magonjwa na magugu.

Mazingira

  •     Hali ya Hewa:

Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa n.k.)

  •     Udongo:

Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 – 7.0.

Aina za Nyanya

Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:

  1. Aina ndefu ( intermediate) kwa mfano ANNA F1, Tebgeru 97. Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji.
    2.Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa)

Kotokana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika makundi mawaili:

  1.     OPV (Open Pollinated Variety) – Aina za kawaida
     2.      Hybrid – Chotara: Hizi ni aina zenye mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu.

Katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema.

SOMA; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo – 2

Kuandaa Kitalu cha Nyanya

Mambo muhimu ya kuzingatia:

  •     Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu
  •     Kiwe sehemu iliyowazi na yenye udongo ulio na rutuba ya kutosha
  •     Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe tambarare au na mwiinuko kidogo ili kuepuka maji yasituame kwenye kitalu, mtelemko ukiwa mkali sana nao sio mzuri kwani husababisha mmomonyoko wa udongo.
  •     Kitalu kiwe sehemu ambayo haikuwa na zao la nyanya au viazi mviringo (au mazao ya jamii ya nyanya k.m. mnavu, biringanya n.k.)
  •     Kiwe sehemu ambayo ni rahisi kupata huduma zote muhimu kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa miche kwenda sehemu nyingine. Pia kurahisisha usambazaji wa miche kwenda sehemu nyingine.

Kuandaa Matuta ya Kusia Mbegu za Nyanya

Aina ya matuta:

– matuta ya makingo (sunken seed bed)

– matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed bed)

– matuta ya kawaida (flat seed beds)

Mambo Muhimu ya Kuzingatia wakati wa Kuandaa Matuta

  •     Tuta liwe na upana kati ya sentimita 90-120, na urefu wowote, [ili mradi muhudumu anaweza kutoa huduma nyingine zote kitaluni bila kukanyaga miche].
  •     Kwatua/lima kina kirefu cha kutosha kiasi cha sentimita 15-20 ili mizizi iweze kusambaa vizuri ardhini.
  •     Choma takataka juu ya kitalu, au funika tuta kwa nailoni, majuma 4-8 ili kuua vimelea vya magonjwa na wadudu.
  •     Wakati wa kuandaa, kitalu, ongeza mbolea aina ya samadi/vunde au mboji kwenye udongo kisha kwatua ili ichanganyike vizuri na udongo.
  •     Changanya kiasi cha debe 1 hadi 2 kila baada ya mita moja (hatua moja) mraba.
  •     Tuta lisiwe na mabonde mabonde au mawe mawe ambayo yanaweza kuzuia usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta, lisawazishwe vizuri ili kuhakikisha usambazaji mzuri wa mbegu na kuepuka mbegu kufukiwa chini mno kiasi ambacho hazitaota.

Faida na Hasara za Matuta yaliyotajwa hapo juu

  1. Matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed beds);

– matuta ya namna hii huruhusu maji, hewa na mizizi kupenya kwenye udongo kwa urahisi zaidi.

– Mazao ya mizizi hupata nafasi ya kutosha kutanuka haraka zaidi

– Matuta haya hayatuamishi maji kama mengine, hivyo hutumika zaidi kwenye maeneo yanayokuwa na mvua mara kwa mara.

Hasara:

o Matuta ya namna hii yana sababisha sana mmomonyoko wa udongo kama hayakutengenezwa vizuri.

   2.Matuta ya makingo (sunken seed beds):

Faida:

  •     matuta haya ni rahisi kutengeneza
  •     hutumika wakati wa kiangazi ili kuhifadhi maji na unyevu
  •     nyevu mdogo unaopatikana ardhini
  •     ni rahisi kumwagilia kwa kutumia maji ya mfereji au bomba
  •     huhifadhi unyevu nyevu kwenye ardhi kwa muda mrefu
  •     huzuia mmomonyoka wa ardhi

Hasara:

    Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye
    mvua nyingi.

    3.Matuta ya kawaida (flat seed beds):

Faida:

  •     ni rahisi sana kutengeneza kwani udongo ukisha kwatuliwa
  •     na kusambazwa mbegu huoteshwa
  •     ni rahisi kutumia eneo kubwa kuotesha mbegu

Hasara:

Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye mvua nyingi.

Kusia Mbegu

  •     Hakikisha ubora na uotaji wa mbegu kabla ya kuzipanda kitaluni (germination test)
  •     Weka mistari kwenye tuta kulingana na ukubwa wa tuta, lakini mistari isiwe chini au zaidi ya sentimita 15-20 toka mstari hadi mstari
  •     Kina cha mistari kisiwe cha kutisha bali kiwe kati ya sentimita 1-2
  •     Matuta yapate maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu. Ni vizuri kutumia chombo cha kumwagilia (watering can).
  •     Mbegu ziatikwe kwenye mistari na zisambazwe vizuri ili kufanikisha usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta. Changanya mchanga laini na mbegu kisha sambaza kwenye mistari iliyoandaliwa kwenye tuta.

Mbegu zinaweza pia kuatikwa kwenye tuta bila mistari, lakini zisambazwe kwa uwiano mzuri kwenye tuta ili kupunguza msongamano. Msongamano husabisha magonjwa ya fangasi kama vile kinyausi (damping off) au ukungu (blight).

  •     Weka matandazo kiasi cha kutosha ambacho hakitazuia kuota kwa mbegu.
  •     Mara baada ya kuatika mbegu, mwagilia maji kiasi cha kutosha kulingana na unyevu nyevu ulioko ardhini

Mambo ya Kuzingatia baada ya kusia mbegu pamoja na Matunzo Kitaluni

  •     Mwagilia maji kwenye kitalu baada ya kuotesha kulingana na unyevu nyevu uliopo kwenye udongo.
  •     Miche yote ikisha ota, ondoa matandazo, kisha weka chanja ili kupunguza mionzi ya jua ambayo inaweza kuunguza miche michanga. (kipindi cha baridi si muhimu sana)
  •     Punguzia miche (thinning) ili ibakie kwenye nafasi ya kutosha. Hivyo miche ibakie kwenye umbali wa sentimita 2.5 – 4. Hii itapunguza magonjwa ya ulemavu na mnyauko, pia itasaidia kupata miche bora na yenye nguvu.
  •     Endelea kumwagilia hadi miche ifikie kimo kinachofaa kuhamishia shambani.
  •     Punguza kiwango cha umwagiliaji maji, siku chache kabla ya kuhamishia miche shambani, yaani siku 7-10.

Kanuni na Mbinu za kuhamisha miche toka Kitaluni kwenda shambani (Transplanting

Rules)

  •     Mwagilia miche masaa machache kabla ya kuhamishia miche shambani ili wakati wa kung’oa miche mizizi ishikamane vizuri na udongo.
  •     Kabla ya kuhamisha miche, mashimo yawe yamekwisha andaliwa katika nafasi zinazo stahili huko shambani.
  •     Miche ihamishwe wakati wa jioni ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na jua.
  •     Kwa ujumla karibu mazao yote ya mboga mboga huwa tayari kuhamishiwa shambani yakiwa na majani kamili kati ya 2-6 pamoja na mizizi mingi iliyostawi vizuri.
  •     Mche lazima uwe na afya nzuri, uwe umenyooka vizuri, hivyo miche yote iliyonyongea au myembamba kupita kiasi isichukuliwe wakati wa kupeleka shambani.
  •     Ng’oa miche kwa uangalifu hasa pamoja na udongo wake kwa kutumia vifaa husika ili mizizi isidhurike.
  •     Miche ihamishiwe shambani mapema mara baada ya kung’olewa toka kitaluni.
  •     Wakati wa kuhamisha miche, uangalifu mkubwa utumike ili kutoharibu miche/mizizi.

SOMA; Haya Ndio Mapinduzi Makubwa Tunayohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Kilimo.

Maandalizi ya Shamba la Nyanya

  •     Shamba la nyanya liandaliwe mwezi 1-2 kabla ya kupanda miche.
  •     Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.
  •     Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia nyanya.
  •     Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita (50-60) x (50-75) kutegemeana na aina au hali ya hewa. Kama ni kipindi cha baridi ni vyema nyanya zikapandwa mbalimbali ili kuruhusu mzungungo wa hewa na kuzuia magonjwa ya fangasi.

Jinsi ya kupanda miche:

  •     Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake
  •     Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.
  •     Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa bustanini.
  •     Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kasha weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua.

Mambo muhimu ya kuzingatia baada ya kuhamishia Miche Shambani

  •     Kagua shamba mara kwa mara ili kujua maendeleo au matatizo yaliyoko shambani mapema
  •     Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini.
  •     Ondoa mimea iliyoshambuliwa na magonjwa au ondoa sehemu zilizoshambuliwa, kisha zifukiwe chini au kuunguza moto.
  •     Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha kwenye nyanya pamoja na kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha mazingira magumu ya wadudu maadui kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea unyevunyevu.

Asante sana